Pages

Thursday, December 30, 2010

GBAGBO AZIDI KUWA KICHWA NGUMU

 Sasa Laurent Gbagbo ameamua kugeuka sikio la kufa lisilosikia dawa. Viongozi watatu wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, marais wa Benin, Cape Verde na Sierra Leone, wanawasili leo mjini Abdijan na ujumbe mmoja tu kutoka jumuiya hiyo: aidha Gbagbo awachie madaraka au akabiliane na nguvu za kijeshi.
Lakini hata kabla hawajafika alipo, tayari Gbagbo ameshasema kwamba hatishiki na kitisho hicho, na badala yake ameonya kwamba jaribio lolote la kumuondoa madarakani kijeshi, litaliingiza eneo lote la Magharibi ya Afrika katika vita.
Ziara ya leo inafanyika siku moja tu, baada ya Gbagbo kupata pigo jengine katika jumuiya ya kimataifa pale ubalozi wa nchi yake mjini Paris, Ufaransa, ulipochukuliwa na wafuasi wa Ouattara, baada ya serikali ya Ufaransa kusema kwamba itamtambua balozi aliyeteuliwa na Ouattara kama mwakilishi halali wa Cote d'Ivoire nchini humo. Balozi aliyekuwa akiiwakilisha serikali ya Gbagbo aliondoka ubalozini hapo bila ya kuleta tabu yoyoteNdani ya Cote d'Ivoire yenyewe hapo jana mgomo uliokuwa umeitishwa na Ouattara ulianza kwa kusuasua nyakati za asubuhi, lakini baadaye ikaripotiwa kwamba ulishika kasi, baada ya habari zake kuenea katika eneo la bandari kubwa mjini Abdijan, na kwa kiasi fulani kuzorotesha shughuli za kibiashara. Mgomo huu ulikuwa na mafanikio zaidi katika maeneo ya mbali na mji mkuu. Na katika kile kinachoonekana kama pigo jengine kwa Gbagbo, Umoja wa Afrika umemteua Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, kuwa mwakilishi wake katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Cote d'Ivoire.
Itakumbukwa kwamba Oginga alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kiafrika kumtaka waziwazi Gbagbo awachie madaraka ili kuinusuru nchi yake na machafuko, na pia alikuwa ni yeye aliyetaka nguvu za kijeshi zitumike dhidi ya Gbagbo ikiwa angelionesha ukaidi.
Ukiacha nchi ya Angola ambayo inamuunga mkono wazi wazi Gbagbo, kwa ujumla Umoja wa Afrika umemtenga na unamtaka kiogozi huyo aondoke madarakani. Hata hivyo, serikali yake inaendelea kuwa na udhibiti wa nchi, kwani vikosi vyake vinashikilia maeneo muhimu kama vile mji mkuu wa Abdijan, ambako vinalaumiwa kwa kufanya mauaji dhidi ya wafuasi wa Ouattara.
Baraza la Mawaziri la serikali kivuli ya Ouattara linafanya kazi zake kutokea hoteli ya Golf mjini Abdijan, huku likilindwa na wanajeshi 800 wa Umoja wa Mataifa, lakini wajumbe wake hawawezi kutoka nje ya uzio wa hoteli, ambako wanajeshi wanaomuunga mkono Gbagbo wamewazingira.  

No comments:

Post a Comment