Aliyekuwa Rais wa Misri, Hosni Mubarak, pamoja na wanawe wawili wa kiume wamekamatwa kwa ombi la waendesha mashtaka wa serikali, ambapo watazuiliwa kwa siku kumi na tano hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.
Taarifa kupitia mtandao wa Facebook wa ofisi ya Mwendesha Mashtaka, inasema kuwa mkuu wa serikali, Abdel Maggid Mahmud, alimamuru kuzuiliwa huko kwa Mubarak na wanawe, kama sehemu ya uchunguzi unaofanywa wa matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya wanamageuzi yaliyofanywa nchini Misri mwezi Januari na Februari mwaka huu.
Maafisa wa usalama wamesema kuwa Mubarak anazuiliwa katika hospitali moja ya eneo la Sharm El Sheikh, iliyo kwenye eneo la mapumziko la bahari ya Sham, baada ya kudaiwa kupata mshtuko wa moyo hapo jana wakati akihojiwa na waendesha mashtaka.Polisi imesema kuwa wanawe wawili, Gamal na A'laa, waliwasili katika gereza la Tora mjini Cairo, ambako sasa kumekuwa kama nyumbani kwa maafisa wengine walioangushwa na pia baadhi ya wafungwa sugu wa kisiasa nchini humo.
Mubarak na wanawe wanachunguzwa kwa tuhuma za kuchochea vurugu dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya kupinga utawala wake yaliyodumu kutoka Januari 25 hadi Februari 11, wakati Mubarak alipolazimika kusalimu amri na kujiuzulu. Kiasi ya watu 800 walifariki wakati wa vurumai hizo.
Awali televisheni ya taifa ya Misri ilisema kuwa familia ya Mubarak inazuiliwa kwa siku 15 kwa ajili ya uchunguzi na walikuwa kwanza wamehojiwa katika eneo la Sharm El Sheikh.
Video zilizowekwa kwenye mtandao wa YouTube zilionyesha kile kilichoonekana kama waandamanaji nje ya mahakama ambako familia ya Mubarak ilikuwa ikihojiwa.
Uchunguzi huo uliamrishwa siku ya Jumapili na mkuu wa mashtaka wa serikali kama sehemu ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na matumizi mabada ya mamlaka.
Familia hiyo ya Mubarak inatarajiwa kuulizwa kuhusu madai kuwa walishiriki katika uhalifu wa dhulma dhidi ya waandamanaji na kusababisha vifo na majeraha kwa baadhi yao.
Waziri wa Sheria, Abdel Aziz Al Guindi, alisema kuwa waendesha mashtaka walikuwa wameanza kumhoji Mubarak na mwanawe Gamal hapo jana, na kwamba mahojiano kuhusu wizi wa mali ya umma hayakuwa yameanza, kwa sababu suala hilo litashughulikiwa na Idara ya Kupambana na Mapato Haramu.
Televisheni ya taifa iliripoti kuwa kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 82 alikuwa amesusia kula au kunywa tangu alipopokea habari jana asubuhi kuwa alipaswa kuhojiwa.
Baada ya kujizulu, Mubarak na familia yake walihamia katika makaazi yao yaliyoko kwenye mji wa kifahari wa Sharm El Sheikh. Kumekuwa na maandamano kila wiki ya kutaka ashtakiwe ambapo maelfu ya watu wamejitosa barabarani na kukabiliana na wanajeshi mapema Jumamosi katika uwanja wa Al Tahrir.
No comments:
Post a Comment