Sir George Kahama
Desemba 9, mwaka huu tunatimiza miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika. Hakika umri wa miaka 50 si umri mdogo. Wengi wamezungumzia changamoto zilizopo wakati tukikaribia siku hiyo ya miaka 50. Sir George Kahama ni kati ya waliokuwemo serikalini kuanzia mwanzo kabisa wa uhuru. Amekuwamo katika serikali zilizofuatia kabla ya kustaafu siasa majuzi. Ufuatao ni uchambuzi wake wa wapi tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.
Ni vigumu kuweza kuorodhesha na kuzungumzia maendeleo yote yaliyopatikana Tanzania katika miaka 50 ya mwanzo baada ya Uhuru katika makala fupi kama hii. Kazi hiyo ni kubwa na inahitaji kutungiwa kitabu na pengine si kitabu kimoja!
Hivyo, katika makala hii nimeainisha maendeleo makuu sita yaliyopatikana kwa kuamini kwamba Serikali itaona umuhimu wa kuandika kitabu hicho kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru ifikapo Desemba 9, 2011.
La Kwanza : Ujenzi wa Taifa huru la Watanzania.
Tulipopata Uhuru Desemba 9, 1961 Tanganyika haikuwa Taifa. Ilikuwa ni nchi tu, ya watu wasiozidi millioni 8 wa makabila takribani 126 na ambao hawakuwa na mawasiliano rasmi ya karibu, wala lugha moja ya kitaifa.
Baadhi ya makabila walikuwa wakiongea Kiswahili kama kwamba lugha hiyo ilikuwa ya kigeni! Tanzania sasa ni Nchi na Taifa kamili huru na imara, yenye umoja, mshikamano, amani na utulivu na mfano wa kuigwa barani Afrika. Ni Taifa kubwa lenye watu zaidi ya milioni 43 wanaongezeka kwa wastani mzuri wa asilimia 2.9 kila mwaka.
Hii leo, Watanzania bila kujali hali halisi ya maisha yao ya kila siku, wanajisikia kuwa huru, wana jeuri ya utu wao, na wanajisikia kuwa sawa na binadamu wengine kokote duniani.
Wakati wa Uhuru na miaka mingi baada ya Uhuru, nchi haikuwa na wasomi wengi wazalendo. Nakumbuka Desemba 9, 1961 Tanganyika ilikuwa na wahitimu wa kiwango cha chuo kikuu 120 tu, wakiwamo wanasheria wawili, wahandisi wawili na madaktari wa binadamu 12.
Sasa Tanzania inao wasomi na wataalamu wazalendo lukuki ambao ndiyo wameshika nafasi zote za ushauri na uamuzi serikalini na katika taasisi nyingi nyeti za kitaifa.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wakuu wa kitaifa waliorithi kiti chake wanastahili pongezi.
Napenda niwashawishi Watanzania wenzangu wakubali ukweli kwamba kwa watu waliotoka kwenye utawala wa kikoloni miaka 50 tu iliyopita, hali hiyo niliyoielezea ni ya maendeleo yasiyo na shaka na msingi mkubwa na madhubuti wa kuweza kuchochea maendeleo makubwa zaidi katika kipindi cha usoni.
Pili : Muungano wa pekee barani Afrika
Nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar kwa hiari, na bila shinikizo la mataifa makubwa ya nje zimeungana na kuwa Taifa moja la Wa-Tanzania. Hili nalo ni tukio jingine kubwa la aina yake barani Afrika.
Muungano huu umepewa na unaendelea kupewa tafsiri nyingi na watu wa ndani na nje ya nchi. Lakini tafsiri mojawapo ambayo haiwezi kuwa na ubishi ni kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeimarisha usalama wa Kitaifa (State Security) wa sehemu zote mbili za Muungano.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Mzee Abedi Amani Karume wanastahili pongezi za dhati za wananchi wote wa Tanzania kwa upeo wao mkubwa wa kuona mbali (their visionary Leadership).
Tatu : Ukombozi wa Afrika
Tanzania ilishiriki kwa hali, mali na damu katika vita na kampeni za ukombozi wa Bara la Afrika. Hii ilitokana na msimamo wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwamba “Uhuru wa Tanganyika hautakuwa na maana kama nchi nyingine za Afrika zitaendelea kutawaliwa na Wakoloni”.
Msimamo huo wa Tanganyika uliungwa mkono kwa dhati na Umoja wa Nchi huru za Afrika wakati huo (OAU) na ambao uliiteua Tanganyika kuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya OAU.
Mchango na Sadaka ya Tanzania vinathaminiwa na kuenziwa na Nchi za Afrika na hasa zile zilizokuwa na kambi kuu za mapambano za vyama vyao vya ukombozi kwenye ardhi ya Tanzania wakati wa mapambano.
Nne : Huduma ya Elimu
Desemba 9, 1961 Tanganyika ilikuwa na Chuo Kikuu kimoja kilichojulikana kwa jina la “The University of Dar es Salaam”, na kikiwa na hadhi ya “The College of the University of London”. Chuo hicho kilianzishwa kwa shinikizo la TANU (Tanganyika National African Union) kikiwa na Wanafunzi wa Sheria 14!
Mwaka 1970 Chuo Kikuu hicho kilipandishwa hadhi ya kuwa Chuo Kikuu cha Taifa na kutangazwa rasmi kama “The University of Dar es salaam”.
Kwa takwimu za mwaka 2010 Tanzania sasa ina Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki visivyopungua 30 (11 vya Umma na 19 vya binafsi) vyenye kusajili wanafunzi zaidi ya 100,000.
Chuo Kikuu kipya cha Dodoma (UDOM) peke yake kina uwezo wa kusajili wanafunzi 40,000 na ni cha pili kwa ukubwa katika nchi za Afrika Mashariki na SADC, (nyuma ya chuo Kikuu cha UNISA cha Pretoria chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 45,000).
Kwa upande wa Elimu ya Msingi Tanzania leo ina shule 15,816. Wakati wa uhuru kulikuwa na wanafunzi 486,470 wa shule za msingi lakini hadi mwaka 2010 kulikuwa na wanafunzi milioni 8.4.
Kuhusu Shule za Sekondari, wakati wa Uhuru kulikuwa na wanafunzi 11,832 wa Sekondari lakini hadi 2010 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.6.
Kuhusu mafunzo ya elimu ya ufundi Tanzania inavyo Vyuo Vikuu vya Ufundi (Technical Colleges) vitano. Viko vile vile vyuo vingi vya ufundi (craft-level) vinavyoendeshwa na taasisi binafsi.
Vyuo vya ufundi vya VETA kwa takwimu za 2010 vilikuwa na usajili wa wanafunzi 125,000.
Kutokana na uzoefu wangu wa miaka mingi nimebaini kwamba maendeleo yoyote ya haraka (crash programmes) katika kila jambo huja na changamoto zake.
Hivyo changamoto zilizojitokeza katika upanuzi wa haraka wa elimu katika ngazi zote zilitarajiwa: Ukosefu wa madawati, upungufu wa vitabu vya kufundishia, upungufu wa walimu wenye sifa zinazohitajika, upungufu katika ubora wa elimu ya wahitimu na kadhalika.
Zote hizi ni changamoto zitokanazo na maendeleo ya haraka na kwa maoni yangu ni bora kuhangaika na changamoto zenye sura hiyo ya maendeleo kuliko changamoto zenye chimbuko katika kutokuwa na mipango yoyote ya maendeleo.
Tano : Huduma za Afya
Desemba 1961, Tanganyika haikuwa na hospitali kubwa za kujivunia mbali na hospitali ndogo ya Sewa Haji ya Dar es Salaam na hospitali ndogo ndogo za Serikali na madhehebu ya dini mikoani.
Hivi sasa tunazo hospitali kubwa za kisasa sita na hospitali kuu za Mikoa na Wilaya. Tunazo vile vile hospitali zinazotoa huduma maalumu za magonjwa ya moyo na ubongo na vile vile zenye hadhi ya chuo kikuu cha taaluma ya matibabu (university hospitals).
Ziko vile vile hospitali na kliniki nyingi ndogo ndogo za binafsi na maduka ya madawa (pharmacies) ya kutosha.
Na tunayo mipango maalumu katika hatua mbalimbali za utekelezaji iliyoanzishwa na Serikali kwa lengo mahsusi la kutokomeza magonjwa sugu ya malaria na ukimwi.
Kutokana na mipango bora ya maendeleo katika Sekta ya Afya umri wa kuishi Mtanzania umeongezeka hadi miaka 58.4 kwa wastani, kwa takwimu za mwaka 2010.
Sita : Miundo mbinu ya barabara.
Mtandao wa barabara nchini Tanzania hadi sasa una jumla ya kilometa 86,472. Barabara zenye lami kwa nchi nzima ni kilometa 6,700 ambapo sehemu kubwa ni ya barabara kuu.
Mikoa yote ya Tanzania Bara imeunganishwa kwa barabara za lami isipokuwa Mikoa minne ya Rukwa, Kigoma, Tabora na Manyara na hiyo itaunganishwa karibuni. Wilaya karibu zote nazo zimeunganishwa kwa barabara za lami na Makao Makuu ya Mkoa.
Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo ikilinganishwa na wakati tunapata Uhuru mwaka 1961 ambapo barabara nyingi zilikuwa za vumbi na hazipitiki wakati wa mvua, kwa mfano, safari kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa gari ilichukua hadi siku 14, sasa ni kati ya saa 12 hadi 16!
Leo hii Mtanzania akiamua afanye hivyo anasafiri kwa barabara ya lami kutoka ama Dar es salaam au Mtwara hadi Mtukula hadi Kigali hadi Johannesburg!
TANZANIA : MIAKA 50 YA UHURU NA CHANGAMOTO ZA USONI
B: SEHEMU YA PILI : CHANGAMOTO ZA USONI
UTANGULIZI :
Enzi za kupigania Uhuru na hata baada ya Uhuru kupatikana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuacha kuwaasa na kuwakumbusha Watanzania kwamba walidai Uhuru ili kuutumia Uhuru huo kuondoa maadui wetu Wakubwa watatu:
Umasikini (Poverty),
Ujinga (Ignorance) na
Maradhi (Disease)
Kama nilivyoelezea katika sehemu ya kwanza ya makala haya, Tanzania katika miaka 50 iliyopita imepiga hatua kubwa za kujivunia katika kupambana na maadui hao. Na wala mafanikio hayo hayakupatikana kwa urahisi hata kidogo!
Kwa nyakati tofauti Tanzania ilikumbana na vikwazo vingi vilivyorudisha nyuma juhudi za maendeleo kama vile ukame, mafuriko, milipuko ya magonjwa, migogoro ya mafuta ya petroli, Vita ya Kagera dhidi ya Idd Amin wa Uganda, kuvunjika kwa Jumuia ya Afrika Mashariki na vita vya ukombozi wa Afrika.
Lakini pamoja na hayo, na bila kubeza mafanikio makubwa yaliyopatikana ni vema pia tukiri kwamba safari yetu ya kufikia lengo letu la kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania bado ni ndefu.
Asilimia 36 ya Watanzania bado hawajaweza kumudu mahitaji yao ya msingi. Asilimia 86 ya wananchi hawapati umeme wa gridi. Na wote tunajua ya kwamba, wananchi wengi bado wanaishi katika nyumba zenye ubora usioridhisha, zilizojengwa kwa kuta za miti, fito na matope na kuezekwa kwa makuti au nyasi. Na kwa ngazi ya kitaifa bajeti ya Tanzania ni tegemezi kwa asilimia 28.2 (Kwa takwimu za 2010).
Watu wanauliza : Kulikoni? Tanzania iliyobarikiwa kwa maliasili nyingi za madini, ardhi kubwa nzuri na yenye rutuba ya kuweza kuzalisha mazao mengi ya biashara na chakula, mito mingi na maziwa, jiografia inayoonewa wivu na majirani, kwa nini bado inahesabika katika kundi la nchi masikini sana duniani?
Swali lililopo mbele ya Watanzania ni hili : Tufanye nini sisi Watanzania, kutatua kitendawili hiki?
Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayotukabiri sote kwa ujumla wetu, kila Mtanzania na kila mzalendo, Serikali, sekta binafsi na vikundi mbalimbali vya kijamii nchini, na pia marafiki wa Tanzania wenye mapenzi mema.
Nionavyo mimi, kitendawili hiki pengine kinaweza kutatuliwa ikiwa tutafanya utafiti wa kina wa kujua ukweli halisi, halafu tukajipanga vizuri zaidi katika kupanga matumizi ya raslimali tulizojaliwa, hususani hizi zifuatazo:
Ardhi (Kwa tafsiri pana)
Nguvu kazi
Jiografia
Mazingira
Nishati za umeme
Na kwa kuwa mipango ya maendeleo ili yafanikiwe yanahitaji uwepo wa utekelezaji makini inabidi vile vile tufanye tathimini ya vyombo vya utekelezaji tulivyoviunda ikiwemo Idara ya Utumishi wa Umma, kujiridhisha kama miundo ya vyombo hivyo na tija yake inakidhi hali ya utandawazi na ushindani mkubwa uliopo katika ulimwengu wa sasa.
Pengine kwa maelezo ya ziada nitumie mfano wa mfumo ulipo wa Idara Kuu ya Utumishi wa Umma (Government Civil Service Structure).
Pamoja na mageuzi (reforms) yaliyokuwa yakifanyika mara kwa mara mwelekeo wa “Civil Service”yetu, kwa maoni yangu umekuwa zaidi wa “udhibiti” badala ya uwezeshaji (facilitative). Mwelekeo huo ndio umezaa na ndio unaendeleza kuwapo kwa urasimu ambao unalalamikiwa sana na Wawekezaji na Wakala (Agents) wengi wa Maendeleo.
Pengine katika hili kuna haja ya kuazima tena uzoefu na ushauri wa nchi ya Ghana kama tulivyowahi kufanya huko nyuma.
Sekta ya Kilimo
Katika miaka 50 iliyopita tumebuni sera nyingi nzuri za kuendeleza kilimo, kama ifuatavyo :
Uhuru na kazi (Wito kwa Watanzania wote).
Kilimo cha kisasa (Agricultural Modernization kwa kutumia trekta, maksai, mbegu bora, mbolea, n.k).
Siasa ni Kilimo.
Vijiji vya Ujamaa.
Kilimo ni uti wa mgongo.
Benki ya kilimo.
Kilimo kwanza.
Pamoja na kuwa na sera hizo nzuri kilimo chetu bado kimeendelea kuwa duni na hivyo kutowasaidia wakulima ambao ndio sehemu kubwa ya Watanzania, kuondokana na umasikini.
Mazao ya biashara na chakula, kama takwimu za miaka 30 iliyopita zinavyoonyesha (isipokuwa zao la mahindi na mpunga) hayajazalishwa kwa wingi wa kutosheleza kumwezesha mkulima mdogo apate kipato cha kumwondoa katika lindi la umasikini.
Limekuwepo pia tatizo kubwa la mazao mengi yanayolimwa na wakulima wadogo kukosa soko la uhakika.
Naamini kwamba tatizo la masoko likipatiwa ufumbuzi mkulima atapata motisha tosha ya kuongeza uzalishaji.
Kwa lengo hilo hilo mbinu zinazotumika kuendeleza sekta ya kilimo kwa ujumla zitabidi nazo zibadilike. Uelekezaji na Usimamizi wa kilimo itabidi ukabidhiwe kwa vyombo zaidi ya kimoja. Pamoja na Wizara ya Kilimo kuendelea na jukumu lake la msingi la kuwa mhimili mkuu wa sekta ya kilimo, vyombo vingine pia kama vile JKT, SUA, na taasisi nyingine zenye mwelekeo wa kilimo itabidi vishirikishwe kila chombo kikiwa na majukumu maalumu.
JKT, kwa mfano, wangeweza kupewa jukumu la kuendeleza zao la zabibu kama zao kuu la biashara katika Mkoa wa Dodoma. Hivi sasa Tanzania ni ya pili, nyuma ya Afrika Kusini katika kilimo cha zabibu lakini si kwa kiwango cha mapato. SUA nao wangeweza kupewa jukumu la kuendeleza kilimo katika Mkoa wa Morogoro na kuufanya uwe kweli ghala la Taifa la mazao ya chakula kwa ajili ya soko la ndani na nje, hususani soko lililopo katika himaya yetu ya Afrika Mashariki na SADC.
Kwa maoni yangu Tanzania inahitaji kutumia mbinu za kimapinduzi (unorthodox methods) ili kukifanya kilimo chetu kiwe chenye manufaa kwa mkulima na kwa Taifa.
Suala la utafiti wa masoko lina umuhimu wa pekee katika mipango yetu ya kilimo. Mazao mengi yanayozalishwa na mengine ambayo yangeweza kuzalishwa nchini Tanzania yanahitajika katika masoko ya nchi za nje na hasa za Afrika Mashariki na SADC kama wafanyabiashara wa nchi hizo watapewa uhakika wa mazao hayo kupatikana kwa kiasi wanachohitaji na kwa ubora na wakati unaotakiwa.
Utafiti uliofanywa na vyombo vya kimataifa umebaini kwamba lipo soko kubwa katika nchi za Afrika kusini mwa Sahara lenye thamani ya takribani dola za kimarekani bilioni 50 la mazao ya vyakula vinavyopendwa sana na Wa-afrika walio wengi kama vile mahindi meupe, ndizi, muhogo, matunda ya kila aina, na kadhalika.
NGUVU KAZI
Tanzania tuna bahati kubwa ya kuwa na vijana wengi wenye shauku na ari ya kufanya kazi. Vijana hawa ni raslimali muhimu sana katika vita ya kupambana na umasikini kama watawezeshwa ipasavyo, kwa mfano, kupatiwa mafunzo maalumu ya uzalishaji mali mbinu sahihi za kuandaa na kuendesha miradi ya kiuchumi na biashara, na kusaidiwa mitaji.
Pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Uwezeshaji bado Tanzania hatujafanikiwa sana katika kubuni mikakati na mbinu sahihi pana za kuwezesha wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Mikakati na mbinu makini inabidi ziandaliwe kwa kushirikisha pamoja vyombo zaidi ya kimoja. Ushiriki wa taasisi kama vile CTI, TCCIA, taasisi za fedha, makampuni makubwa ya ujenzi na ya biashara, viwanda, mashamba makubwa ya kilimo, vyuo vikuu na kadhalika, ni muhimu sana.
Nitataja mifano miwili ya fursa za ushirikishwaji. Katika sekta ya ujenzi wako vijana wengi wanaotengeneza matofari. Vijana hao wangeweza kuunganishwa na makandarasi na makampuni ya ujenzi kwa mikataba kwa kupewa miongozo na mafunzo. Vijana watapata ajira za uhakika pamoja na teknolojia ya kisasa, na makandarasi pengine nao watapata vifaa vya bei nafuu.
Fursa nyingine ni ya vijana wanaotengeneza samani. Hao nao wakiwezeshwa na kuelekezwa vizuri wanaweza kutengeneza samani madhubuti zaidi kuliko zile zinazoagizwa kutoka nchi za nje ambazo ubora wake ni wa shaka. Fursa nyingi za namna hii pia zinaweza kuandaliwa kwa kushirikisha wenye mashamba makubwa ya kilimo na mifugo.
JIOGRAFIA YA TANZANIA
Jiografia tuliyojaliwa Tanzania ni kitega uchumi chenye uhakika wa kuweza kuleta maendeleo ya ki-uchumi kama kikitumiwa kwa ujasiri. Tumezungukwa na nchi sita zinazotegemea ardhi ya Tanzania kupitishia biashara zao. Nchi hizi zikiunganishwa na bandari zetu kwa barabara nzuri za lami, reli, mabomba ya kusafirishia mafuta na vile vile viwanja vya ndege vya kisasa, mapato ya Tanzania ya fedha za kigeni kutokana na malipio ya kutumia huduma hizo yanaweza hata yakawa makubwa zaidi kuliko yale yatokanayo na mauzo ya mazao ya kilimo nchi za nje.
Serikali inastahili pongezi kwa kuliona hili na kuanzisha mchakato wa kulifanyia kazi.
MAZINGIRA
Utunzaji makini wa mazingira ni jambo muhimu katika jitihada zetu za kuondoa umasikini. Tuna misitu mingi mizuri ambayo inasaidia katika upatikanaji wa mvua, malighafi za ujenzi, samadi, na kadhalika. Maziwa makubwa ya Afrika yamo ndani ya mipaka yetu.
Hivyo basi inabidi Serikali iweke mikakati madhubuti ya utunzaji makini wa raslimali hizi tulizojaliwa.
Kwa bahati mbaya tumeanza kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira ukifanyika bila Serikali kubuni mikakati makini ya kuudhibiti. Uharibifu huu ni ule wa ufyekaji hovyo wa misitu kutafuta kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na biashara.
Takwimu zilizopo zinathibisha kwamba biashara ya kuni na mkaa inasababisha uvunaji wa hekta 300 za misitu kila siku. Uharibifu huu unatisha na usipodhibitiwa ipasavyo utafanya sehemu kubwa ya Tanzania kugeuka jangwa katika miaka michache ijayo. Matokeo yake yatakuwa ni kuongezeka na si kutoweka kwa umasikini.
Uwezekano wa kupata nishati mbadala upo. Moja ni kuwa na viwanda vya kutengeneza “briquette” (mkaa wa kiwandani) kama wanavyofanya Uchina. Mbadala mwingine ni kuwashawishi wananchi watumie gesi na mafuta ya taa (kerosene) kwa kuondoa kodi zilizowekwa.
NISHATI YA UMEME
Kwa nchi yoyote ile umeme ni ufunguo mkuu (master key) wa maendeleo ya kiuchumi hususani viwanda, vituo vikuu vya biashara, na migodi ambavyo, pamoja na kuzalisha bidhaa vinaajiri wafanyakazi wengi na hivyo kutoa fursa nyingine ya kupunguza umasikini.
Matatizo ya umeme yanayoikabili Tanzania hivi sasa yanajulikana na yametokana kwa kiasi kikubwa na suala la uzalishaji wa umeme kutopewa kipa-umbele stahiki katika miaka ya nyuma.
Pengine hatukuwa na uhakika kama Tanzania ingeweza kuwa na mvuto mkubwa kwa wawekezaji wa kitaifa kama ule tulioushudia katika miaka ya karibuni.
Na kwa bahati mbaya washauri wetu wakuu kama vile Benki ya Dunia waliegemea zaidi kwa mfumo wa kuzalisha umeme wa maji (hydro-power), kwa kisingizio cha gharama nafuu za uzalishaji. Hawakuishauri Tanzania mapema kutumia pia vyanzo vingine tulivyo navyo kama vile makaa ya mawe, gesi asilia, mionzi ya jua na kadhalika.
Kutokana na mafunzo tuliyoyapata inatubidi sasa kama Taifa suala la umeme tulipe ki-paumbele nambari moja! Na hatua zichukuliwe bila urasimu usio wa lazima katika kuchukua hatua zinazohitajika. Ukiritimba uliopo katika uzalishaji (production), usafirishaji (transmission) na usambazaji (distribution) wa umeme nao uangaliwe upya.
Na ikiwezekana tuwe na wizara pekee (The Ministry of Energy) yenye jukumu moja tu la kuhakikisha umeme wa kutosha unapatikana wakati wote.
USHIRIKISHWAJI WA WATAALAM WAZALENDO
Tanzania tunavyo vyuo vikuu vingi na vyuo hivyo vina wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali. Lakini kwa maoni yangu raslimali hii nayo kwa kiasi fulani hatujaitumia ipasavyo katika harakati za kitaifa za kutatua matatizo yetu ya ki-uchumi hususani katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na utafutaji wa mbinu sahihi za utekelezaji.
Wakati umefika kwa Serikali ya Tanzania kutumia dhana ya kuwa na Mabaraza ya Ushauri (Independent Council of Advisors) kama mbinu mojawapo ya kutumia Utaalamu na Uzoefu mwingi uliopo nchini mwetu!
HITIMISHO
Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere baada ya Tanganyika kutimiza miaka 10 ya Uhuru aliwakaribisha maofisa wa kikoloni waliotumika Tanganyika waje kushuhudia maendeleo yaliyopatikana chini ya Uongozi wa Viongozi wa Tanganyika huru kulinganisha na yale ya miaka 80 ya ukoloni wa Wajerumani na Waingereza.
Maafisa hao walitembezwa katika sehemu zote za Tanganyika na hawakuweza kuamini macho yao kwa maendeleo ya kusisimua waliyoyaona.
Waliporudi Dar es salaam, Mwandishi mmoja (kutoka Nigeria) aliyefuatana na maofisa hao alimuliza Rais Nyerere swali lifuatalo :
“Mr. President, what can you tell us has been your biggest achievement?
Haieleweki Mwandishi huyo alikuwa na lengo gani, lakini alipewa jibu alilostahili, lifuatalo :
“We survived”.
Jibu alilotoa Rais Nyerere lilionekana wakati huo kama ni la utani! Lakini katika dunia ya kesho sote tunakoelekea suala la “survival” si la utani tena!
Tanzania itakumbana na ushindani mkali katika kusaka ajira, katika kufanya biashara, katika kutafuta watalii, katika kutafuta wawekezaji, na kadhalika. Ushindani huo utaanzia ndani ya nchi na utaenea katika Jumuiya zetu za SADC na Afrika Mashariki na ulimwenguni kote.
Hivyo basi inabidi Watanzania tujiandae, tujinoe, na kujipanga vizuri, kukabiliana na ushindani huo mkali kuanzia sasa (au jana?), kila Mtanzania na kila mzalendo popote aliko.
No comments:
Post a Comment