UJUMBE wa viongozi kutoka nchi tatu za Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) umekwenda Ivory Coast kuzungumza
kwa mara ya mwisho na rais aliyemaliza muda wake Laurent Gbagbo, kuachia madaraka. Habari zilisema ujumbe huo ni wa viongozi wa nchi za Benin, Sierra Leone na Cape Verde ambao waliwasili jana mjini Abidjan, kwa ajili ya kumshawishi Gbagbo kukabidhi madaraka kwa kiongozi aliyeshinda uchaguzi, Alassane Outtara. ECOWAS katika mkutano wake wa hivi karibuni uliofanyika Abuja, Nigeria, ilitishia kutumia nguvu kumuondoa madarakani Gbagbo, ikiwa atakataa kuondoka kwa njia ya amani. Wakati ECOWAS ikiendelea na juhudi zake, Umoja wa Afrika umemteua Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, kuwa mjumbe wake maalumu katika kushughulikia mgogoro huo.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa walisema uteuzi wa Odinga ni pigo lingine kwa Gbagbo, kwakuwa Odinga alikuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kutoa msimamo wa kutumika nguvu za kijeshi dhidi ya Gbagbo. Hata hivyo Odinga alisema amepanga kuzungumza na Gbagbo, lakini uamuzi wake wa mwisho utategemea na matokeo ya mazungumzo kati ya Gbagbo na viongozi wa ECOWAS.
Mwaka 2008, Odinga alitangazwa kuwa waziri mkuu wa Kenya katika serikali ya umoja wa kitaifa, baada ya kuibuka mzozo wa matokeo ya uchaguzi wa urais na kusababisha mgogoro wa kisiasa nchini humo. Hata hivyo Odinga alisema kuwa uwezekano wa kuwa na serikali ya kugawana madaraka nchini Ivory Coast haupo, kwakuwa tume ya uchaguzi ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza mshindi na siyo mahakama ya katiba.
Wakati huo huo taarifa kutoka Abidjan zilisema wafanyakazi wengi wa mji huo waliupuuza wito wa kushikiri katika mgomo wa nchi nzima, uliotolewa na kiongozi wa upinzani Alassane Outtara, anaetambuliwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo. Taarifa zilisema kazi ziliendelea kama kawaida kwenye bandari muhimu za Abidjan na San Pedro, zinazotumika kusafirishia zao la kakao. Maduka yalifunguliwa na watu walienda maofisini.
No comments:
Post a Comment