Pages

Wednesday, December 29, 2010

WAZIRI MAKANGA AKIRI MAPUNGUFU KATIKA SHERIA YA KAZI


 WAGENI wengi kutoka nchi mbalimbali wanafanya kazi zinazoweza kusimamiwa na Watanzania, kutokana na upungufu uliopo katika
Sheria za kazi. Hatua hiyo inawafanya waajiri katika kampuni binafsi, kutowapatia watanzania fursa hizo kwa kuwa sheria haziwabani. Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa idara mbalimbali katika wizara hiyo mkoani Mara. Hatua ya Dk. Mahanga imekuja kufuatia Ofisa Kazi wa Mkoa huo, Venance Kadago, kudai kuwa kampuni binafsi zimeajiri wageni kwa mikataba bila kupata vibali kutoka wizarani.
Alisema kila wanapofanya ukaguzi, hukutana na tatizo hilo ambalo alidai linasababishwa na vibali wanavyopewa wageni vinavyowapatia fursa ya kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa. Alisema upungufu uliopo katika sheria unatoa mwanya kwa maofisa uhamiaji nchini, hasa waliopo mikoani, kutoa vibali kwa wageni vinavyowaruhusu kufanya kazi maalumu. Hata hivyo, Dk. Mahanga alisema vibali hivyo vimekuwa vikitolewa bila kuihusisha wizara husika, kitu ambacho alisema ni hatari kwa taifa.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mahanga alisema wizara yake ina mpango wa kufanya marekebisho ya sheria za kazi ambazo zitaainisha taratibu za wageni kuishi na kufanya kazi nchini. Pia, alisema marekebisho hayo yatasaidia kuondoa mgongano wa majukumu baina ya Wizara ya Kazi na Idara ya Uhamiaji nchini.
“Tumeingia katika utandawazi na ushirikiano wa kiuchumi, biashara na ajira, hivyo si busara kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania wakapewa wageni,” alisema. Dk. Mahanga alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Idara ya Uhamiaji nchini kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira, katika masuala ya ajira kwa wageni hasa wakati huu sheria inapoonyesha upungufu.

No comments:

Post a Comment