Kura ya maoni ya Jumapili huko Sudan Kusini inawapa wapiga kura nafasi ya kuchagua kama wanataka kubaki kuwa nchi moja au kuwa taifa linalojitegemea.
Kura hiyo inatokana na mkataba wa amani wa mwaka 2005 ambao ulimaliza miaka 21 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Sudan Kaskazini na Kusini.
Wapigakura wanaoingia katika vituo vya kupiga kura wataona alama mbili. Moja inaonyesha mikono miwili ikiungana pamoja, ikimaanisha umoja. Alama nyingine inaonesha kiganja kimoja cha mkono, ikimaanisha kujitenga.
Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanabashiri watu wa kusini watachagua kuwa taifa huru. Taifa hilo jipya litakuwa la kwanza barani Afrika tangu Eritrea ilipopata uhuru mwaka 1993.
Ili kufanya hatua hiyo kuwa tulivu, hata hivyo Kaskazini na Kusini watatakiwa kutatua masuala kadhaa muhimu ikiwemo mipaka, haki za raia, maji na zaidi ya yote ni suala la mafuta.
Pande zote bado hazijakubaliana juu ya namna ya kugawana mapato kutoka rasilimali huko kusini ambazo zinazalisha kiasi cha mapipa nusu milioni ya mafuta kwa siku.
Makubaliano ni muhimu kwa sababu wakati Kusini inazalisha mafuta, mabomba ambayo yanaongoza kusafirisha mafuta nje ya nchi yanapita Kaskazini.
Pande hizo pia zinabaki kugawanyika juu ya mzozo wa eneo la Abyei linalozalisha mafuta. Abyei awali ilipangiwa kufanya kura tofauti ya maoni siku ya Jumapili, kama inataka kuungana na Kaskazini au Kusini. Lakini kura haikutekelezwa kwa sababu ya migogoro juu ya nani atastahili kupiga kura.
No comments:
Post a Comment