Pages

Tuesday, May 1, 2012

MALARIA BADO NI TATIZO DUNIANI KOTE


Ni hakika kwamba ubinaadamu umetiwa hatarini kwa kuzingirwa na Malaria. Katika maeneo yote ya kitropiki, vimeenea vimelea vya ugonjwa huo vinavyohatarisha afya ya mwanaadamu na kusababisha vifo vya kiasi ya watu milioni moja hufa kila mwaka duniani. Ilipotangazwa tarehe 25 Mai na Shirika la Afya Duniani kuwa siku ya kimataifa ya Malaria, dhamira ilikuwa ni kutoa tahadhari kwamba ugonjwa huo upo na unayakata maisha yetu.
Wataalamu wanasema kwamba Malaria huanza na homa yenye baridi kali sana na aghlabu humalizikia kwa kuviathiri vibaya viungo vya mwili na hata kifo. Nusu ya wanaokufa kutokana na ugonjwa huu ni watoto wadogo, anasema daktari Kai Braker, anayeongoza Mradi wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka, huku eneo la Afrika lililo kwenye mstari wa Ikweta, likiwa limeathirika zaidi.
"Daktari katika mataifa hayo kila siku huona wagonjwa wengi wakiendelea kuzidi kuwa na hali mbaya. Wengi wao huwa watoto wenye upungufu mkubwa wa damu na ambao wanapumua kwa tabu. Na hilo linashitusha sana." Anasema Daktari Braker.
Umasikini kikwazo cha mapambano

Sindano kwa ajili ya Malaria nchini Kenya.
Sindano kwa ajili ya Malaria nchini Kenya.
Wanaoshituka zaidi ni wale ambao hawana madawa ya kuukabili ugonjwa huo, maana dawa mchanganyiko za kutibu malaria zinafanya kazi vizuri zikitumiwa vyema, lakini ni mpaka kwanza ziwepo. Umasikini unapokuwa umewagubika watu na Malaria ikaja juu yake, huwa kuna machache yanayoweza kufanywa kuokoa maisha yasipotee. Daktari Braker anasema kwamba umasikini na malaria ni pande mbili za sarafu moja.
"Ni kama vile pana mduara wa papo kwa papo: ukiwa masikini una uwezekano mkubwa wa kupata Malaria. Maana katika jamii zenye umasikini, watu wanakuwa hawana elimu ya kutosha kujikinga na maradhi hayo na wala mahala ambapo wanaweza kupata matibabu. Kwa upande mwengine, ugonjwa wa malaria unaondoa nguvu kazi na unadhoofisha uwezo wa jamii kuzalisha kwa maendeleo yao."
Mazalia ya mbu

Unyunyizaji wa dawa ya kuulia mbu majumbani
Unyunyizaji wa dawa ya kuulia mbu majumbani
Kupambana na na kufanikiwa kuuangamiza ugonjwa wa Malaria, kunatokana pia kuyaangamiza mazalio ya mbu. Vita dhidi ya ugonjwa huo, kwa hivyo, ni vita dhidi ya mdudu: mbu aitwaye Anophelis. Kupambana na mdudu huyu ni jambo linatalo rasilimali na teknolojia, ambayo nayo pia inakosekana kwenye mataifa masikini.
Daktari Jürgen May wa Taasisi ya Bernad-Nocht inayojihusisha na madawa ya nchi za tropiki mjini Hamburg, anasema mara tu mdudu huyo akidhibitiwa kikamilifu, dunia inaweza kujitangazia ushindi kwenye vita hivi vigumu.
"Asiyeumwa na mbu, hawezi kupata malaria. Kwa hivyo, hapa ndipo linapokuja suala la umuhimu wa kutumia vyandarua na hatua nyengine za kuzuia kuumwa."
Chandarua kinaweza kukaa hata mwaka mzima bila ya kutoboka, lakini mbu mmoja hawezi kuishi ndani ya kipindi chote hicho. Anapokuwa ametaga mayai yake kwenye madimbwi au mahala popote, mayai hayo yanapasa kuangamizwa kwa madawa.
Licha ya madawa yanayotumika kwa kazi hiyo, kama ile DDT, kuthibitika kuwa na athari mbaya kwa mazingira, katika siku za karibuni Shirika la Afya Duniani, WHO, limeidhinisha matumizi ya DDT, likisema kwamba kama ikitumika vyema, basi haina madhara kwa binaadamu na wanyama.
Juu ya yote, kwa mataifa masikini, bado hadithi inaendelea kubakia kuwa ile ile ya vipi wanaweza kuigharamikia teknolojia ya kinga na tiba ya Malaria; na vipi wanaweza kuwakinga watoto wao wasiumwe na mbu wa Anophelis, na hatimaye kuugua malaria, ambayo hupelekea vifo vya watoto hao.

No comments:

Post a Comment